Thursday, 31 October 2019


MFAHAMU ANNIE


Jina lake rasmi ni Annie Odeka. La msimbo ni Lollipop. Hili la msimbo alilipata wakati akiwa mjamzito. Rafiki zake waliishia kumwita Lollipop kutokana na kasumba yake ya kukivamia kitamu hicho alipokuwa mama mtarajiwa.
Hapendi kutaja umri wake kwa kuwa anaamini ati huwenda watu wengi wakakosa kumwamini. Isitoshe, ana imani thabiti kuwa huzidi kuwa mchanga kadiri miaka inavyosonga mbele. Kwa hivyo, ni sahali zaidi kwa mwenye uchu huu kuziangalia picha za Bi Annie, nazo zitasaidia kuudhihiri umri wake.
Annie ni binti mrembo na bashashi sana. Ucheshi na uchangamfu wake mwingi huelekea kuichosha misuli ya mashavuni kila anapoipa dunia yake tabasamu.
Ngozi yake ya mwili imekoleza weusi wa kuridhisha, kupendeza na kuvutia. Cheusi dawa hasa, ukipenda.
Amejaaliwa afya ya miguu. Afya impayo utata wa kupata viatu vya kufu ya miguu yake. Haikosi yeye ni miongoni mwa watu ambao hulazimika kufanya maagizo maalum ya viatu kwenye maduka ya viatu.
Kimo cha kiwiliwili chake ni futi 5`6.
Hashabikii mtindo mmoja tu wa nywele zake. Hujaribu mfumo wowote uwao ule, alimradi unamchukua barabara.
Binti huyu mrembo ni shabiki ashiki wa tojo na ndiyo sababu ametojwa jina la mtu ampendaye zaidi hapa duniani. Utamfahamu tu. Annie anafahamisha kuwa zipo tojo nyingine kadhaa atakazotiwa kando na hiyo iliyoko kwenye maeneo ya karibu na bega lake la shimali.
Kwa sasa, Annie anaishi mjini Nairobi. Ni mpenzi mkubwa wa vitabu na fasihi. Ghashi huyu anaazimia kuliwahi jukwaa la uanahabari katika siku za halafu, panapo majaliwa. Huba yake ya uandishi imemfikisha kwenye kilele cha kufanya machapisho kwenye blogu zake mbili;
Annie Odeka si binti wa madaha sana wala mhitaji sana. Huridhishwa na mambo madogo madogo ya maishani kama vile kushiriki mlo na wenziwe na kufurahikiana. Vile vile, unapotia nia kumzawidi dada huyu, usijichoshe na gharama kubwa kubwa. La! Zawadi ya thamani ndogo sana huweza kufanya kweli. Anathamini furaha na utu. Utu wa kweli.
Aghalabu, Annie hupenda vitu vya kumfikirisha sana. Vitu vya kulipa kazi bongo lake. Haitoshi hivyo tu! Anaamini uwepo wa mazingaombwe na mazingira ya sampuli hii.
Miongoni mwa vitu anavyovikumbatia sana ni kama vile;
  • Televisheni na vitabu (hukosa raha anapoikosa sauti ya runinga chumbani. Hali sawa na anaposoma.)
  • Sinema za vitushi na vichekesho
  • Wageni wachangamfu na wangwana
  • Miziki ya kale
Vitu asivyovipenda ni kama;
  • Watu wasioridhika na walichonacho
  • Majina mabaya na ya matusi
  • Visa vinavyoisha na huzuni (vya runingani na vitabuni)
Vyakula anavyovipenda ni;
  • Chapati (kwa kuwa mamake alikuwa hodari wazo)
  • Samaki ( labda kutokana na asili yake ya kiluo)
  • Yogurt
  • Crisps
Annie anaipenda rangi ya buluu. Anaamini kuwa rangi hii ni ya amani.
Annie anampenda nani? Mwanawe! Tojo aliyonayo ni ya jina la huyu mwanawe.
Kwenye mtandao wa twitter, anapatikana kwa jina @odeka_annie

No comments:

Post a Comment